Daish

Kuhusu mungu wa kike wa Misri ya Kale, angalia Isis Daish (pia Daesh, tamka: da-ish au da-esh, kwa Kiarabu داعش, kifupisho cha ad-Dawlah al-Islāmiyah fīl-ʿIrāq wash-Shām yaani Dola la Kiislamu katika Iraq na Shamu); maarufu pia kama IS, na awali ISIL au ISIS (kutokana na tafsiri ya Kiingereza Islamic State) ni kundi la Waislamu wenye itikadi kali lililoteka na kutawala kwa muda maeneo mbalimbali ya Iraq, Syria, Yemen, Libya, Nigeria na kufanya kazi katika nchi nyingine 14, zikiwemo Afghanistan na Pakistan. Hadi Desemba 2017 ilitawala sehemu kubwa za Iraq, hadi Machi 2019 sehemu za Syria mpaka kuondolewa kijeshi na kulazimishwa kuendelea kwa siri. Tarehe 29 Juni 2014 kundi hilo lilijitangaza kuwa ukhalifa (khilāfah) wa kimataifa chini ya Abu Bakr al-Baghdadi na kwa sababu hiyo kupunguza maneno fīl-ʿIrāq wash-Shām (ya Iraq na Syria) katika jina lake kuwa الدولة الإسلامية, ad-Dawlah al-Islāmiyah tu. Kwa msingi huo linadai mamlaka ya kidini, ya kisiasa na ya kijeshi juu ya Waislamu wote duniani, likitangua uhalali wa mwingine yeyote. Bila shaka, Waislamu walio wengi, hasa wenye mamlaka za namna hizo, hawalikubali. Umoja wa Mataifa unalaumu Daish kwa makosa ya jinai dhidi ya utu, kama vile mauaji ya kimbari na dhuluma za kidini, hasa dhidi ya Wakristo na Wayazidi, lakini pia dhidi ya Waislamu wenye msimamo tofauti, kwa namna ya pekee Washia. Kwa sababu hiyo UN unaliona kundi la magaidi tu, na nchi zaidi ya 60 ziko vitani dhidi yake kwa namna moja au nyingine. Daish inajulikana kwa matumizi yake makubwa ya vyombo vya habari na mawasiliano hata katika kutangaza mambo inayofanya kinyume cha taratibu za kimataifa, kama vile kuua kikatili raia na kubomoa sehemu za Urithi wa Dunia. Makao makuu yalikuwa Ar-Raqqah, Syria.


© MMXXIII Rich X Search. We shall prevail. All rights reserved. Rich X Search